Usafi mwisho wa Mwezi waendelea Kata ya Mnadani
Na. Coletha Charles, DODOMA
Wananchi wa Kata ya Mnadani
Halmashauri ya Jiji la Dodoma walifanya usafi wa mazingira mita tano kuzunguka
maeneo yao ya makazi na biashara ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya serikali
ya kila Jumamosi ya mwisho wa Mwezi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo
la usafi, Mkuu wa Kitengo cha Usafi na Usimamizi wa Taka ngumu Halmashauri ya
Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro, alisema kuwa ni wajibu wa viongozi kuhamasisha
jamii juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kufanya kazi kwa pamoja na
wananchi.
Alisema kuwa wananchi wanatakiwa
kujiepusha na utupaji wa taka ovyo katika maeneo na kufanya usafi katika mitaro
ambayo inapitisha maji machafu kipindi hiki cha mvua nyingi na kujiepusha na
mafuriko yatokanayo na uzibaji wa mitaro. “Usafi ni ustaarabu ambao
unaanza na mimi na wewe. Lakini katika kipindi hiki cha masika, kumekuwa na
changamoto ya magonjwa mbalimbali ya kuhara na kutapika ambayo tunaweza
kujiepusha kwa kufanya usafi kwenye maeneo yetu” alisema Kimaro.
Nae, Mkazi wa Mtaa wa Mailimbili, Mwadawa Omary,
alimesa kuwa kila mwanajamii ana jukumu la kuhakikisha mazigira yanayo mzunguka
yanakuwa safi kwa kushirikiana wanaweza kuboresha afya na ustawi wa jamii. “Usafi
ni sehemu ya imani yetu na tunaposhirikiana, tunaweza kufanikisha malengo yetu
ya kufanya maeneo yetu kuwa safi na salama. Ninaiomba halmshauri iwachukulie
hatua watu ambao hawajitokezi kufanya usafi katika maeneo yao” alisema Omary.
Usafi wa Mazingira ni hatua ya
kutekeleza maagizo ya serikali kuwa halmashauri zote nchini kila mwisho wa mwezi
ziweze kufanya usafi kwaajili ya kuyatunza na kuweka mazingira safi na salama
kwa ubora wa afya.
MWISHO
Comments
Post a Comment