Wananchi washauriwa kusikiliza elimu na hamasa ya Dodoma Jiji Mtaa kwa Mtaa Uchaguzi Festival
Na. Asteria Frank, DODOMA
Wananchi
wameshauriwa kujitokeza kwa wingi kusikiliza elimu inayotolewa na wahamasishaji
kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa njia mbalimbali ikiwemo kikundi maalum
cha ngoma cha Dodoma Jiji Mtaa kwa Mtaa Uchaguzi
Festival.
Afisa Utamaduni wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Desdery Kuzenza akihamasisha mamia ya wananchi wa Swaswa Mnarani |
Hayo,
yalisemwa na Afisa Utamaduni wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Desdery Kuzenza alipokuwa
akihamasisha wananchi kujitokeza kutumia haki yao ya msingi na ya kikatiba ya
kupiga kura na kuwachagua viongozi watakaowafaa kwa manufaa ya maendeleo ya
mitaa yao. “Naomba nitoe rai kwa wakazi wa Dodoma na maeneo mbalimbali waendelee kushiriki katika ‘program’
mbalimbali za elimu kwa umma ambazo zinalenga kuwaelimisha kuhusiana na umuhimu
wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na nafasi za uongozi wa serikali za mitaa
katika maisha yao ya kila siku na tunasema kwamba serikali za mitaa kwa sauti
ya wananchi. Hivyo, wajitokeze kupiga kura kwa maendeleo ya mitaa yao na
karibuni kushiriki katika tamasha hili la
Dodoma Jiji Mtaa kwa Mtaa Uchaguzi Festival” alisema Kuzenza.
Aidha,
mmoja wa wasanii katika kikundi cha DOTI, Salum Ramadhani alisema jukumu lao
kubwa ni kuwaelimisha wananchi kuhusiana na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
hususani tarehe 27 Novemba, 2024 wajitokeze kwa wingi kwenye kupiga kura
kwaajili ya kumchagua kiongozi atakaewaongoza mtaani kwao. “Sisi ni wanakikundi
wa DOTI, tumeanzia kuzunguka maeneo mengi sana katika mitaa ya Dodoma mjini kama
Swaswa mnarani, Ntyuka, Nkuhungu Boda, Mwatano na sehemu mbalimbali kwa lengo
la kuwahimiza wananchi wajitokeze kupiga kura kwa njia ya maigizo na ngoma”
alisema Ramadhani.
Akipongeza
juhudi zinazofanywa na Dodoma Jiji Mtaa kwa Mtaa Uchaguzi Festival, mkazi wa Kata ya
Ntyuka, Maige Paul, alisema amefurahi ujio wa Mtaa kwa Mtaa Uchaguzi Festival na hiyo inaonesha kwamba wananchi
wote tunatakiwa kwenda kuchagua viongozi wanaounda serikali za mitaa akiwemo mwenyekiti
na wajumbe wake watano. “Mtaa kwa Mtaa inaendelea kutufurahisha lakini pia inaendelea
kutuhamasisha kwamba, jukumu linalofata ni kubwa ambalo tunatakiwa kwenda
kuchagua viongozi ambao watatuletea maendeleo katika kata zetu pamoja na mitaa
yetu” alisema Paul.
Akiongelea
kuhusu wananchi kujitokeza kupiga kura, mkazi wa Kata ya Ntyuka, Latifa Hamadi
alitoa rai yake kwa wakina mama na vijana ambao wana sifa za kupiga kura
kujitokeza kwa wingi siku ya kuchagua viongozi na kushauri elimu hii isiishie
mtaani kwao tu bali ifike na sehemu nyingine. “Nawaomba wakina mama na vijana
waliofikisha miaka 18 waende kupiga kura inapofika tarehe 27 Novemba, 2024. Tumependa
ujumbe tuliopata katika hamasa hii, lakini pia nawashauri waende kata nyingine
nyingi za Jiji la Dodoma kama Kata ya Kilimami, Mkonze na Hazina” alisema Hamadi.
Tamasha
la uhamasishaji la Jiji la Dodoma Mtaa
kwa Mtaa Uchaguzi Festival linafanywa kwa njia ya kitamaduni na sanaa mbalimbali kwa
kutumia maigizo, uchezeshaji ngoma za asili na wasanii nguli wakitumbuiza
katika mitaa nyakati za mchana, jioni na usiku ili kuwafikia wananchi wote wakiwa mitaani
kwao na kwa wale wanaoshinda kazini wakirudi waweze kupata burudani pamoja na
ujumbe wa elimu ya umuhimu wa kuchagua viogozi watakaoongoza katika mitaa yao.
MWISHO
Comments
Post a Comment