Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uwazi mtupu Jiji la Dodoma
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
UCHAGUZI wa Serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Jiji
la Dodoma unafanyika kwa uwazi kwa mujibu wa kanuni zilizopo ili wananchi
wafurahie kukua kwa demokrasia.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko
Kauli hiyo ilitolewa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa mwaka 2024 Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko
alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu mwenendo na shughuli
mbalimbali za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zinazoendelea ofisini kwake leo.
Dkt. Sagamiko alisema kuwa hakuna mpango wowote wenye
nia ovu ya kuminya demokrasia kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa viongozi wa
mamlaka za serikali za mitaa. Alisema kuwa tangu mchakato wa Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa unaanza ulikuwa wa wazi na shirikishi ukiruhusu vyama vyote kushiriki
kikamilifu.
Akiongelea zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za
kugombea nafasi za uongozi alisema kuwa vyama vyote 19 vilishiriki zoezi hilo
katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Halmashauri ya Jiji la Dodoma tunajivunia
mafanikio haya ya kidemokrasia. Vyama 15 ndivyo vimechukua na kurudisha fomu
kwa nafasi mbalimbali za uongozi” alisema Dkt. Sagamiko.
Akiongelea upotoshaji unaofanywa kwenye mitandao ya
kijamii kuhusu mipango inayopangwa kuengua baadhi ya wagombea kutoka moja ya
chama cha siasa alisema kuwa hakuna mipango hiyo. Alisema kuwa hakuna uteuzi wa
wagombea uliofanyika hadi itakapofika tarehe 8 Novemba, 2024. Aidha, aliwata
wananchi kuwapuuza wale wote wanaotaka kuleta taharuki katika jamii kwa kutoa
taarifa za upotoshaji. “Sisi kwa umoja wetu, siyo tu tuzipuuze taarifa hizo za
upotoshaji bali kuendelea kutoa elimu. Kuendelea kuwasisitiza wananchi kufuata kalenda
ya matukio ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa
uwazi ilibandika orodha ya wapiga kura ili watu waweze kuhakiki usahihi wa
taarifa hizo.
Comments
Post a Comment