Chigongwe watakiwa kujitokeza kupiga kura
Na. Dennis Gondwe, CHIGONGWE
WAKAZI wa Kata ya Chigongwe, Halmashauri ya Jiji la
Dodoma wameshauriwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwenye Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa tarehe 27 Novemba, 2024 ili waweze kuwachangua viongozi wanaowafaa.
Masima Masima (wa pili kushoto) wakati wa kuhamasisha umma
Kauli hiyo ilitolewa na mkazi wa Kata ya Chigongwe,
Masima Masima alipokuwa akiwahamasisha wananchi wa kata hiyo kujitokeza siku ya
kupiga kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa alipopata nafasi ya
kuhamasisha wakati timu ya uhamasishaji ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilipofika
katani hapo kutoa hamasa kwa wananchi.
Masima alisema “mimi binafsi cha kwanza, kupiga kura
ni jukumu langu na ni haki yangu ya msingi. Tarehe 27 Novemba, mwaka huu ni
siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Tunakwenda kumchagua mwenyekiti na
wajumbe wake, mimi Masima nipo tayari kushiriki uchaguzi huo”.
Kwa upande wa mkazi mwingine wa kata hiyo, Salome
Nguji alisema kuwa wanachohitaji wapate kiongozi bora siyo viongozi wa mchongo
ili wawasaidie. “Tunahangaika na maji, zahanati na shule. Mwenyekiti na wajumbe
wa serikali ya mitaa watusaidie. Hivyo, nina wahimiza tujitokeze kwenye kupiga
kura hiyo tarehe 27 Novemba, 2024” alisisitiza Nguji.
Wakati huohuo, wafanyabiashara wa Kata ya Chigongwe walisema
kuwa wapo tayari kujitokeza siku ya kupiga kura na kuwachangua viongozi
wanaowahitaji.
Zoezi la kupiga kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
linatarajia kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024 chini ya kaulimbiu isemayo “Serikali
za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi”.
MWISHO
Comments
Post a Comment