RC Senyamule afafanua uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura
Na. Asteria Frank, DODOMA
Mkuu wa Mkoa Dodoma, Rosemary Senyamule ametoa
ufafanuzi wa dhana mbalimbali kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura
unaoendelea katika Wilaya ya Dodoma, Chamwino, Bahi na Kongwa.
Mkuu wa Mkoa Dodoma, Rosemary Senyamule
Kauli hiyo aliitoa alipokuwa mbele ya vyombo vya
habari leo katika ukumbi wa mkutano ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuhusu juhudi za
kuelimisha wananchi wa Mkoa wa Dodoma kuhusu mchakato wa uboreshaji wa daftari
la kudumu la mpiga kura unaoendelea katika Wilaya ya Dodoma, Chamwino, Bahi, na
Kongwa.
Alisema “napenda kutoa ufafanuzi kuhusu dhana
mbalimbali zilizojengeka miongoni mwa wananchi. Kuna taarifa zisizo sahihi
zinazozungumziwa kuhusu gharama za uandikishaji, muda wa vitambulisho vya
kupiga kura na mchakato wa uboreshaji daftari la kudumu la mpiga kura”.
Aliongeza kuwa uboreshaji taarifa za wapiga kura ni
bure, wananchi hawatakiwi kulipa pesa yeyote katika mchakato huo. Dhana ya
kwamba kuna gharama zinazohusiana na
uandikishaji ni dhana za uongo na zinapaswa kupuuzwa.
“Pili, vitambulisho vya kupigia kura, tunatoa
ufafanuzi kwamba vitambulisho vilivyo tolewa hapo awali ni vitamulisho halali
na vinaweza kutumika tena. Hivyo, basi wananchi waliojiandikisha huko nyuma
hawapaswi kuhofia kuwa vitambulisho vyao vimekwisha muda wake, na hawahitaji
kujiandikisha tena ili wapate vitambulisho vipya. Tatu, kuhusu alama za vidole
ni muhimu kujua kwamba wakishachukuliwa alama za vidole hivyo, katika
uandikishaji wa awali hawaitaji kuchukuliwa tena, alama za vidole
zilizochukuliwa nyuma zilezile zitabaki kuwa halali na zitaendelea kutumika na
hii nazungumzia kwa wale wapiga kura waliokuwa halali na hawajabalisha vituo na
wala hawana taarifa yeyote ya kubadilisha” alisema Senyamule.
Akitoa ufafanuzi kuhusu uhusiano kati ya uboreshaji wa
daftari la kudumu la mpiga kura na uchaguzi wa serikali za mtaa, alisema Mkuu
wa Mkoa “mchakato wa uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura ni kwaajili
ya uchaguzi wa mwaka 2025. Unafanywa kwaajili ya kuhakikisha kuwa kila mtanzania
mwenye haki ya kupiga kura, anapata nafasi ya kumchagua diwani, mbunge na rais.
Haina uhusiano wa moja kwa moja na uchaguzi wa serikali za mtaa japo tunajua
katika mfumo wa uongozi, huu ndio mfumo wa chini wa uongozi kwa nchi yetu. Uchaguzi
wa serikali za mtaa una taratibu zake za uandikishaji ambazo zilishatangazwa na
waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa yaani Ofisi
ya Rais (TAMISEMI), ambae ni Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa”.
Alitoa wito kwa wananchi wote kuwa na uelewa sahihi kuhusu
mchakato huo. Alishauri kufuata taratibu zinazotolewa na mamlaka husika ili
kuhakikisha wanatimiza haki yao ya kikatiba.
“Na kwamba ili kupata taaria sahihi ama maelezo
wanaweza kuwasiliama na viongozi wao wa vitongoji, vijiji, mitaa, kata au waratibu
wa uandikishaji ambao wapo kwenye kila halmashauri. Aidha, wanaweza kutembelea
tovuti rasmi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambayo ni www.inec.go.tz. Takwimu sawa
kuhusu idadi ya wapiga kura Dodoma inakadiriwa kuwa na wapiga kura 1,777,834, kati
hao, ambao hawajawahi kujiandikisha kwenye daftari ni 845,976. Aidha, napenda
kuwafahamisha wananchi kuwa vituo vya kuandikisha wapiga kura ni vingi. Hivyo, wasiwe
na hofu, kwamba watatumia muda wao mrefu vituoni. Katika Wilaya ya Dodoma tuna
vituo 429, Wilaya ya Bahi tuna vituo 191, Wilaya ya Kongwa tuna vituo 229 na
Wilaya ya Chamwino tuna vituo 805” aliongeza.
MWISHO
Comments
Post a Comment