Magereza wapongezwa kupambana na ukatili wa kijinsia
Na. Valeria Adam, DODOMA
Waziri, Dkt. Gwajima awapongeza wanawake wa
Jeshi la Magereza Tanzania kwa kupambana na kuzuia changamoto za ukatili wa
kijinsia ili wanawake wachangie katika maendeleo ya taifa.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima akifungua mkutano mkuu wa kwanza wa Mtandao wa Wanawake wa Jeshi la Magereza Tanzania
Pongezi hizo zilitolewa na Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima
alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa kwanza wa Mtandao wa Wanawake wa Jeshi la
Magereza Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa Mtakatifu Peter jijini Dodoma.
“Hatua hii inaonesha ni jinsi gani sera na
miongozo mbalimbali ambayo serikali inatoa kuhusu kufikia usawa wa kijinsia
katika maeneo mbalimbali nchini, inavyotekelezwa kwa vitendo. Na ninyi mmegeuza
miongozo na sera kuwa vitendo kwa kuratibu nchi nzima wanawake katika jeshi
hili la Magereza.
Utekelezaji huu ambao umenigusa pia ni kwa
sababu una ajenda inayohusu kabisa wizara hii ninayoiongoza ambayo ni ajenda ya
kipaumbele ya kupambana na kutokomeza ukatili wa kijinsia, unyanyasaji,
udhalilishaji kwa wanawake na watoto katika kazi mbalimbali nchini. Ajenda hii
nimeibeba vilivyo na ajenda hii niwaambie kwamba imepokelewa vizuri"
alisema Dkt. Gwajima.
Akitoa maelezo ya kina kuhusu mtandao huo kwa
mgeni rasmi, Mkuu wa Gereza la Kongwa, SP. Tecla Ngilangwa alisema kuwa mtandao
huo umepata mafanikio makubwa. "Dhumuni la mtandao, kwanza ni kuwawezesha
wanawake kujitambua, kujiamini, kuthubutu na kujithamini. Pili kuongeza ujuzi
na weledi wa wanawake kupitia mafunzo, sekta na makongamano ili waweze
kushiriki katika fursa mbalimbali kwa manufaa ya jeshi na jamii. Tatu ni kukuza
usawa wa kijinsia na kuimarisha uhusiano kati ya wanawake na mwisho kuhakikisha
uwepo wa uwakilishi wa wanawake kiutendaji na kitaalamu ndani na nje ya jeshi kwa
kadri inavyowezekana" alisema SP. Ngilangwa.
Aliongeza kwa kusema kwamba mtandao huo
haujaweza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa kutokana na changamoto mbalimbali,
lakini kuna baadhi ya mafanikio waliyoyapata. “Mafanikio tuliyoyapata ni
wanawake kujituma na kufanya kazi kwa bidii na weledi wa hali ya juu. Mengine
ni kuongezeka kwa ujasiri kwa watumishi wa kike katika kukabiliana na
changamoto zinazowakabili maeneo ya kazi bila kuvunja sheria, kanuni na
taratibu za mahali walipo. Pia kuongezeka kwa ari na uthubutu wa kutekeleza
majukumu mbalimbali ambayo kabla ya mtandao huu hayakufikiriwa kuwa yanaweza
kufanywa na watumishi wa kike kwa ufanisi mkubwa" alifafanua SP.
Ngilangwa.
MWISHO
Comments
Post a Comment