Mbunge Mavunde kuwekeza zaidi sektan ya Elimu Dodoma

 

Na. Dennis Gondwe

Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde ameahidi kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu ili kuwawezesha wanafunzi wa Dodoma kusoma vizuri na kufikia malengo yao.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri akitoa salamu za Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini


Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alipokuwa akitoa salamu za Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini katika mkutano wa wadau wa elimu Wilaya ya Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa Shule ya St. Gasper jijini Dodoma.

Alhaj Shekimweri alisema “Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini anasema kuwa nitaendelea kuwekeza zaidi kwenye elimu ili kuwasaidia watoto wa Dodoma kufikia malengo yao. Nitashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuinua na kuboresha elimu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma hasa katika miundombinu na mazingira rafiki ya kusomea”.

Akiongelea mapinduzi katika teknolojia, alisema kuwa Dodoma inaelekea kupiga mapinduzi makubwa kwenye elimu. “Dunia inakwenda kwenye mapinduzi makubwa ya teknolojia, lazima tutumie maendeleo hayo katika kurahisisha ufundishaji wa wanafunzi. Ni jambo la msingi sana. Ukifika pale shule ya sekondari Dodoma utaona serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Ofisi ya Rais, Tamisemi na Taasisi ya Elimu Kibaha na wafadhili imewekeza mfumo wa ‘e-learning’ na Shule ya Sekondari Dodoma ni miongomi mwa shule 10 zinazofanyiwa majaribio. Mwalimu akiwa Kibaha mkoani Pwani au Dodoma anaweza kuwa darasani kufundisha wanafunzi wa darasa lake, wanamuona na kufundisha wanafunzi wa shule nyingine na kumuona na kuuliza maswali na kujibiwa” alisisitiza Alhaj Shekimweri.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo alisema kuwa kila mdau wa elimu ana nafasi katika mafanikio ya sekta ya elimu. 

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo akielezea lengo la mkutano huo


“Sote tupo hapa na tunahusika moja kwa moja kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu bora. Hivyo, tutajadili tulipo na jinsi ya kuendelea mbele na namna ya kutatua changamoto za elimu. Tunajua serikali ya awamu ya sita imefanya mambo makubwa na kuweka msingi utakaowasaidia watoto wetu na taifa letu kusonga mbele katika maendeleo na kuboresha huduma za kijamii. Katika kuunga mkono juhudi hizo, leo tutatoa tuzo kwa walimu waliofanya vizuri katika shule na majukumu yao, lakini pia wapo wanafunzi ambao wamefanya vizuri katika masomo yao. Hiyo itakuwa chachu kwa wengine kufanya vizuri zaidi.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma