CCM Mkoa yaipongeza Dodoma Jiji kuondoa migogoro ya Ardhi
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI
ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma imeipongeza Halmashauri ya
Jiji la Dodoma kwa dhamira yake ya kuondoa migogoro ya Ardhi na kuwaondolea
kero wananchi.
![]() |
Donald Mejiti (MNEC) akiongea na wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa, Kamati ya Fedha na Utawala ya Jiji la Dodoma na Menejimenti ya Jiji la Dodoma |
Pongezi
hizo zilitolewa na kiongozi wa kamati hiyo Donald Mejiti alipoongoza Kamati ya Siasa
ya CCM Mkoa wa Dodoma katika ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo
katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mejiti
alisema “tunatoa pongezi za dhati kwako Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma na Mkurugenzi wa Jiji kwa kuonesha nia ya dhati kupunguza na kuondoa
kero kwa wananchi inayotokana na migogoro ya Ardhi katika Halmashauri ya Jiji
la Dodoma. Maoni yetu Chama Cha Mapinduzi ni kwamba mkishapima maeneo wekeni
utaratibu mzuri wa kuyalinda ili yasivamiwe. Kuna tabia ya wananchi kuvamia
maeneo yaliyopimwa na kumilikishwa kialali kwa wananchi na kung’oa ‘beacon’.
Mwananchi mwenye eneo anapokwenda kuangalia au kulinda eneo lake hufukuzwa kwa
mapanga na kutishia amani. Utaratibu huu utawaondolea usumbufu wananchi halali
wanaodhulumia haki zao”.
Kwa
upande wa Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pilly Mbaga alitoa pongezi kwa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma kulipa fidia na kutatua migogoro ya Ardhi. Alisema kuwa awali
wananchi walikuwa wakienda kwa wingi katika ofisi za CCM kulalamikia migogoro
ya Ardhi na madai ya fidia, idadi hiyo imepungua sana siku hizi. Aidha,
alishauri kuwa maeneo ambayo hayajapimwa na halmashauri yaweze kupimwa ili
kuondoa uwezekano wa kuvamiwa.
Katika
hatua nyingine Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo
alisema kuwa wananchi waliotakiwa kulipwa fidia walikuwa 385 ikiwa ni
utekelezaji wa mkakati wa kumaliza migogoro ya Ardhi. “Wananchi 127 ndio
walijitokeza kulipwa fidia. Rai yangu hao wananchi waliobaki wajitokeze ili
waweze kulipwa” alisema Kayombo.
Akiongelea
viwanja mbadala, alisema kuwa halmashauri ilikuwa na deni la viwanja mbadala
3,992. Viwanja 1,102 vimetolewa kwa wananchi na viwanja 2,890 bado wananchi
wanadai ambavyo watapatiwa kufikia mwisho wa mwezi Februari, 2024.
Kamati
ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dodoma imefanya ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo
katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya miaka 47
ya kuzaliwa kwa CCM.
MWISHO
Comments
Post a Comment