JIJI LA DODOMA KINARA MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2023
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI
ya Jiji la Dodoma imeibuka kinara katika mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023
iliibuka nafasi ya kwanza kimkoa, kikanda na nafasi ya pili kitaifa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule (wa kwanza kushoto) akikabidhi cheti cha mshindi wa kwanza wa Mwenge wa Uhuru ngazi ya Mkoa na Kanda Jiji la Dodoma |
Taarifa
hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alipokuwa akitoa
maelezo mafupi kuhusu matokeo ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 katika
kikao cha mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya na watendaji katika mkoa na
halmashauri kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma.
Senyamule
alisema kuwa mwaka 2023 Mkoa wa Dodoma ulikuwa mkoa wa 30 kabla ya mkoa wa
kilele kukimbiza Mwenge wa Uhuru. “Wakimbiza Mwenge wa Uhuru wanakuwa na vigezo
wanavyoangalia hasa wanaangalia fedha zilizoletwa zimetumikaje, ubora wa miradi
iliyoletewa fedha na Mheshimiwa Rais imesimamiwaje kwa tija na ufanisi kiasi
gani na kuona jinsi ambavyo tumehamasisha wananchi kupokea ujumbe wa Mwenge wa Uhuru
ambao ni ujumbe wa kitaifa kwa lengo la kuongeza umoja na mshikamano kitaifa”
alisema Senyamule.
Alisema
kuwa mkoa ulipokea barua kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana, Kazi na watu
wenye Ulemavu ikionesha matokeo ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 kwa kila
halmashauri, kimkoa, kikanda na kitaifa.
“Niseme
mambo machache katika Mkoa wa Dodoma halmashauri tano zimeingia katika 10 bora.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeshika nafasi ya kwanza kimkoa, nafasi ya
kwanza kikanda na nafasi ya pili kitaifa” alisema mkuu wa mkoa.
Halmashauri
nyingine zilizoingia 10 bora ni Halmashauri ya Mji Kondoa imeshika nafasi ya
pili kimkoa, nafasi ya pili kikanda na nafasi ya sita kitaifa. “Halmashauri ya Wilaya
ya Mpwapwa imeshika nafasi ya tatu kimkoa, nafasi ya tatu kikanda na nafasi ya
nane kitaifa. Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa na Kongwa zimefungana zikiwa
nafasi ya nne kimkoa, nafasi ya nne kikanda na nafasi ya 10 kitaifa” alisema
Senyamule huku akibubujikwa na tabasamu la wazi.
Alisema
kuwa matokeo hayo yamepelekea Mkoa wa Dodoma kufikia asilimia 83.54 ya ufanisi
kwenye shughuli za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023. “Dodoma mwaka 2022 tulishika
nafasi ya 22 kitaifa jambo hilo halikutufurahisha, tulipeana shime kuwa hiyo
siyo nafasi yetu kama mkoa. Kutokana na matokeo hayo na juhudi mbalimbali
zilizofanyika mwaka huu kwa mara ya kwanza katika historia ya Mkoa wa Dodoma,
Mkoa wa Dodoma umeshika nafasi ya kwanza kitaifa” alisema Senyamule kwa furaha.
![]() |
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule (katikati) akifurahia ushindi na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri (kushoto) na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, John Kayombo (kulia) |
Ikumbukwe
kuwa kikao cha mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya na watendaji katika mkoa na
halmashauri kiliongozwa na mkuu wa mkoa, kikihudhuriwa na Kamati ya Usalama Mkoa,
Katibu Tawala Mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa mamlaka za serikali za
mitaa, waratibu wa Mwenge wa Uhuru na maafisa wengine waandamizi wa serikali.
MWISHO
Comments
Post a Comment