SERIKALI YAANZISHA KLINIKI YA ARDHI DODOMA KUTATUA KERO ZA WANANCHI


Na. Dennis Gondwe, DODOMA

SERIKALI imeanzisha kliniki maalum ya Ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya serikali ya awamu ya sita.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Ally Gugu alipotembelea siku ya kwanza ya utekelezaji wa majukumu ya kliniki hiyo na kuongea na mamia ya wananchi waliojitokeza katika eneo la iliyokuwa Halmashauri ya Manispaa ya zamani jijini hapa.

Gugu alisema “hii ni kliniki maalum ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma akishirikiana na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma na Katibu Tawala Msaidizi anayehusika na Miundombinu akiiwakilisha Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma. Lengo ni kuwasikiliza na kutambua kero zenu kwenye masuala ya Ardhi katika Jiji la Dodoma. Tumekuja kuwasilikiza tutambue kero zenu na wananchi wanaotaka kuhakiki maeneo yao na hati miliki tuweze kuwapatia”.

Alisema kuwa kliniki hiyo inaashiria dhamira ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Ardhi na Mkoa wa Dodoma katika kuwahudumia wananchi. “Ndani ya wiki moja tutahakikisha tumetatua changamoto zenu kama tutaona baada ya kujitathmini kama kuna haja ya kuendelea na zoezi hili litakuwa endelevu. Kwa wingi huu wa wananchi tumeona tuwe na eneo kubwa ili tuweze kuwashughulikia kwa wingi. Sisi tuwashukuru sana kwa uvumilivu na kujitokeza kwenu mmekuwa mkishughulikiwa kwa utulivu. Tunaomba uvumilivu wenu uendelee na sisi kama watumishi wa umma ambao Mheshimiwa Rais ametuelekeza tupo tayari kuwasilikiza na kuwahudumia” alisema Gugu.

Kwa upande wake Noel Bismark mwananchi aliyekwenda kupata huduma katika kliniki hiyo alisema kuwa utaratibu ule ni mzuri kwa sababu una uwazi na uwajibikaji tofauti na maafisa wanapofanyika kazi katika ofisi zao.

Kilini ya Ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilianza tarehe 16 mwezi huu na itaendelea hadi tarehe 20 mwezi huu.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma