KLINIKI YA ARDHI JIJI LA DODOMA YAHUDUMIA WANANCHI 3,056 NDANI YA SIKU 5
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KLINIKI
ya Ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma imehudumia wananchi 3,056
waliokuwa na kero za muda mrefu kuhusiana na sekta ya Ardhi yakiwa ni mafanikio
makubwa kwa wananchi wengi kuhudumiwa
kwa muda mfupi.
![]() |
Mkurugenzi wa Jiji, John Kayombo |
Takwimu
hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo
alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake.
Kayombo
alisema “zoezi hili limetoa matokeo chanya kwa ujumla. Wananchi 3,056
walisikilizwa. Hati 1,474 zilitolewa papo hapo. Maombi mapya ya hati 561
yalipokelewa, namba za malipo 1,674 zilitolewa, viwanja 645 vilipandishwa
kwenye mfumo, migogoro ya ardhi 774 ilisikilizwa, wananchi 149 walipata huduma
za Mipango Miji na wananchi 221 walipata huduma za upimaji” alisema Kayombo.
Akiongelea
kliniki hiyo, alisema kuwa ililenga kutatua changamoto za Ardhi kwa haraka. “Zoezi
hili ni sehemu ya hatua za utekelezaji wa mkakati wa Mkoa wa Dodoma wa kumaliza
changamoto za Ardhi. Kwa mujibu wa mkakati huo zoezi hili nimepangwa kuwa
endelevu na litafanyika kwa muda wa wiki moja kwa kila mwezi. Mwezi Oktoba
lilianza tarehe 16-20, 2023 katika Ofisi ya Manispaa ya zamani. Aidha, lengo ni
zoezi hili kuendeshwa katika ofisi za Tarafa zote nne zilizopo Dodoma” alisema
Kayombo.
Mkurugenzi
huyo alisema kuwa huduma mbalimbali zinazohusu sekta ya Ardhi zilitolewa. Huduma
hizo ni “utoaji wa Hati milki kwa haraka, kusikiliza kero za Ardhi na kuzitafutia
ufumbuzi, kutoa elimu ya masuala ya Ardhi pamoja na kurahisisha ulipaji wa kodi
ya pango la Ardhi” alisema.
Zoezi
la Kliniki ya Ardhi liliandaliwa ma Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa
kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maebdeleo ya Makazi kupitia Ofisi ya
Ardhi Mkoa kwa lengo la kuwafikia wananchi wenye changamoto za Ardhi katika
Jiji la Dodoma kwa kutoa huduma zote za Ardhi katika eneo moja.
MWISHO
Comments
Post a Comment