WAKAZI WA DODOMA WASHAURIWA KUPIMA UDONGO KABLA YA KILIMO
Na. Dennis Gondwe, NZUGUNI
WAKAZI wa Halmashauri ya Jiji
la Dodoma wametakiwa kujenga utamaduni wa kupima afya ya udongo ili kujua
mahitaji ya virutubishi kwa udongo vitakavyosaidia kupata mazao mengi na bora.
Mkuu wa Divisheni ya Kilimo Mjini, Yustina Munishi
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu
wa Divisheni ya Kilimo mjini katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Yustina
Munishi alipokuwa akiongelea umuhimu wa afya ya udongo kwa mkulima katika
kuzalisha mazao bora na yenye tija.
Munishi alisema kuwa kujua
afya ya udongo ni muhimu sana kwa mkulima. “Napenda kuwataarifu kuwa kujua afya
ya udongo ni muhimu sana kwa mkulima kabla ya kuanza kilimo alichokusudia. Kujua
afya ya udongo kunamuwezesha mkulima kujua kiasi cha nyongo au tindikali kilichopo
katika udongo. Ukijua afya ya udongo utajua ni zao gani uzalishe na linahitaji
virutubisho gani na uweke mbolea ya aina gani na kwa kiasi gani ili uweze kupata
mazao yaliyo bora. Hii ni muhimu kwa sababu watu wengi wanadanganyika kwa kuona
udongo mweusi anasema hapa kuna mbolea, lakini hatupimi afya ya udongo kwa
kuangalia sura na rangi ya udongo. Tumekuja na seti nzima ya upimaji afya ya udogo
katika Banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwenye maonesho haya ya Nanenane”
alisema Munishi.
Nae Emiliana Waitu aliyetembelea
banda la maonesho la Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema kuwa amewahi kusikia
kuwa udongo huwa unapimwa lakini hakuwa akijua sababu za kupima udongo. “Leo nimeshangaa
kuona vifaa vya kupimia udongo na kuelezwa manufaa ya kupima udongo kabla ya
kuanza kilimo. Kweli teknolojia imeongezeka na Jiji la Dodoma limetuletea mambo
mazuri kwenye maonesho ya Nanenane mwaka huu” alisema Waitu.
Maonesho ya shughuli za
wakulima Nanenane mwaka 2023 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Vijana na
wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula”.
Baadhi ya wataalam wa Divisheni ya Kilimo mjini wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma
MWISHO
Comments
Post a Comment