RC Senyamule alipongeza Jiji la Dodoma kupata Hati safi ya Hesabu za mwaka 2021/2022
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI
ya Jiji la Dodoma imepongezwa kwa kupata Hati safi ya ukaguzi kwa hesabu
zilizoishia tarehe 30 Juni, 2022 na kuupa heshima Mkoa wa Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule akitoa maelekezo katika Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani Jiji la Dodoma kupitia na kujadili ripoti ya CAG |
Pongezi
hizo zilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule aliposhiriki Mkutano
Maalum wa Baraza la Madiwani wa kupitia na kujadili hoja za halmashauri
zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika
ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Mstahiki
Meya naomba nitumie nafasi hii kwa namna ya pekee na kwa idhini yako Mstahiki
Meya kuipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kupata Hati safi ya ukaguzi
kwa hesabu zinazoishia tarehe 30 Juni, 2022. Hongera sana. Hati hii safi ya
ukaguzi inalifanya Jiji la Dodoma kuendelea kupata Hati safi kwa miaka minne
mfululizo kuanzia mwaka 2017/2018. Kitendo hiki kimelipa heshima Jiji la
Dodoma, kimeupa heshima Mkoa wa Dodoma na taifa kwa ujumla kwa kweli mmetupa
heshima wote” alisema Senyamule kwa furaha isiyo kifani.
Akiongelea
chachu ya mafanikio ya Jiji la Dodoma katika ukaguzi huo alisema ni ushirikiano
uliopo. “Mstahiki Meya, mafanikio haya makubwa yanatokana na uwepo wa
ushirikiano chanya baina yenu waheshimiwa madiwani, watendaji wa halmashauri,
viongozi na wadau mbalimbali. Hivyo, nawasihi endeleeni kudumisha ushirikiano
huo ili kuiwezesha halmashauri kuendelea kupata Hati safi katika kaguzi zote
kila mwaka kama ambavyo imekuwa utamaduni wenu. Ni matumaini yangu kuwa
mtautumia ushirikiano huu kuhakikisha hoja zote za ukaguzi zilizotolewa na
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na mkaguzi wenu wa ndani
zinashughulikiwa ipasavyo ili ziweze kuhakikiwa na kufungwa kwa kuzingatia
sheria na taratibu za serikali” alisisitiza Senyamule.
Mwenyekiti
wa mkutano huo maalum Prof. Davis Mwamfupe alisema kuwa Rais, Dkt. Samia Suluhu
Hassan ameelekeza taasisi kufuata maagizo na kanuzi zinavyoelekeza katika
matumizi ya fedha za serikali. “Mheshimiwa Rais akaenda mbali zaidi na kututaka
hesabu zetu ziwe waziwazi na masuala ya kiutawala. Hatuna budi kumpongeza.
Ukiangalia mwenendo wa hizi hoja bado tunahitaji msisitizo. Halmashauri ya Jiji la Dodoma hatuna budi
kujisifia na kujipongeza, kwamba bajeti ikiongezeka na kufikia hata bilioni 150
na zaidi ungetemea makosa yawepo zaidi na hivyo, hoja kuongezeka… lakini wakati
bajeti yetu inakwenda juu, sisi idadi ya hoja inakwenda chini, kwa nini
tusijipongeze katika hili” alihoji Prof. Mwamfupe.
Mstahiki Meya, Prof. Davis Mwamfupe akiongea katika Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani kupitia na kujadili ripoti ya CAG |
Awali
akiwasilisha taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa
mwaka ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, Francis Kaunda alisema kuwa wakati taarifa hiyo inatoka halmashauri
ilikuwa na jumla ya hoja 54. Alisema kuwa kati ya hoja hizo, hoja 21 zilikuwa
za miaka ya nyuma na hoja 33 zilikuwa za mwaka wa fedha 2021/2022.
“Baada
ya majibu ya hoja hizo kuwasilishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali na uhakiki kufanyika hoja 21 zilifungwa na kusalia na hoja 33. Katika
ukaguzi wa hesabu za mwaka wa fedha 2021/2022 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali ametoa Hati safi kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Hati hii
inafanya Jiji la Dodoma kuendelea kupata Hati safi toka mwaka 2016/2017 hadi
mwaka 2021/2022 mfululizo” alisema Kaunda.
Akiongelea
taarifa ya utekelezaji wa maagizo ra Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za
Mitaa (LAAC), alisema kuwa halmashauri ilikuwa na maagizo 10. Maagizo manne
yametekelezwa na maagizo sita yanaendelea kutekelezwa. “Pamoja na taarifa hii
fupi, nimeambatisha hoja zinazoendelea na utekelezaji, maoni ya Mkaguzi, majibu
ya Menejimenti, maoni ya Kamati ya Ukaguzi na maoni ya Kamati ya Fedha na
Utawala, kwa ajili ya kuzipokea, kuzijadili na kutoa maoni na mapendekezo”
alisema Kaunda.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Francis Kaunda akiwasilisha taarifa |
Mkutano
maalum wa Baraza la madiwani utekelezaji wa maelekezo ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI
kuwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu za
mwaka 2021/2022 iwasilishwe na kujadiliwa na Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani
mara baada ya kupokelewa.
MWISHO
Comments
Post a Comment