Wenyeviti wa mitaa Dodoma wahimizwa kutoa huduma bora

Na. Halima Majidi, MTUMBA

Wenyeviti wa mitaa jijini Dodoma wametakiwa kutambua na kusimamia majukumu yao ipasavyo kwa kuwapatia huduma bora na kuwashirikisha wananchi katika miradi mbalimbali ili kuleta tija katika ulinzi na utunzaji wa miradi hiyo.




Hayo yalisema na Mwezeshaji wa Mafunzo ya Uongozi na Utawala bora, Mwinyipembe Victor, wakati akitoa mafunzo hayo kwa wenyeviti wa mitaa yaliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali Mtumba.

Victor alisema kuwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ndogo ya 146 dhumuni la kuwepo kwa serikali za mitaa nikupeleka madaraka kwa wananchi, hivyo wenyeviti wa mitaa wanatakiwa kukumbuka na kutekeleza madaraka yao. “Wenyeviti wa mitaa tumekuwa tunajisahau sisi tunakuwa mabosi halafu wananchi wanakuwa wanahangaika, mwananchi atahangaika ndani ya miaka mitano ambayo umemnyanyasa ila ipo siku na wewe utahangaika” alisema Victor.

Aidha, aliwasitiza wenyeviti wa mitaa kutowaacha nyuma wananchi badala yake kuwachukulia kama wao ndio waajiri wao kwa kutekeleza dhamana zao ikiwemo kuwatumikia na kuwahudumia ipasavyo. “Lengo la kuwashirikisha wananchi katika miradi ya maendeleo ni  kutengeneza ari ya umiliki, mwananchi akishirikishwa katika kupanga hata kwenye kulinda na kutunza lazima atatekeleza tu, serikali ya mtaa itafanya vizuri endapo  mwananchi atapewa madaraka yake” alisisitiza Victor.

Sanjari na hayo aliongeza kuwa moja ya majukumu ya serikali ya mtaa ni kuhakikisha utekelezaji wa sheria za ulinzi wa wananchi pamoja na kuwepo kwa demokrasia katika mitaa. Pia kazi ya serikali ya mtaa ni kuhakikisha wanasimamia taratibu zote zinazohusu mpango mji.

“Kuna sheria inayohusu urembeshaji miji hatuwaambii tu wananchi kuwa wapake rangi ili mtaa upendeze hapana ni sheria inatutaka tuwe na utaratibu wa kuhakikisha mitaa yetu inapendeza na kwa hapa Dodoma tumeanzisha utaratibu wa kuezeka bati la rangi fulani ni kwaajili ya mtaa fulani. Haya yote ni majukumu ya serikali za mitaa” aliongeza Victor.

Nae, Mwenyekiti wa Mtaa wa Sogeambele, Kata ya Chihanga, Meshack Joseph, alisema kuwa anashukuru kwa mafunzo kwasababu yamemfundisha kuwa na weledi katika shughuli anazotakiwa kuzifanya. Pia yamemjengea uwezo wa kujiamini katika utendaji wa kazi. “Kwasababu sehemu nyingine tulikuwa tunafanya kwa kupapasa papasa kwa kujua kwamba nikifanya hiki nitakuwa nimekosea lakini kumbe baadhi ya mambo tulikuwa tunaenda sawa lakini tulikuwa tunaenda kwa kutojiamini. Hivyo, mafunzo haya yametujengea uwezo wa kujitambua, kama mwenyekiti majukumu yangu ni yapi” alisema Joseph.

Alifafanua kuwa katika mafunzo hayo alijifunza sehemu kubwa kuhusu namna ya kuwashirikisha wananchi wake katika masuala mbalimbali yanayohusu mtaa wake ikiwemo utoaji wa maamuzi. “Katika utekelezaji wa mambo yangu, cha kwanza kabisa nikufanya taratibu za kuwashirikisha wananchi wangu katika maamuzi ya mambo yote ninayotaka kwenda kuyafanya kwenye mtaa wangu na pia nitaangali taratibu nyingine za kuibua miradi mbalimbali kwa manufaa ya wananchi wangu” alifafanua Joseph.

Upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyumba 300 Nzuguni, Donata Zitatu alisema kuwa, amefurahi sana kwa mafunzo hayo, kwasababu yamemuwezesha kujua mipaka yake na utendaji kazi kama mwenyekiti pamoja na kusimamia mtaa wake, pia amejifunza namna ya kuanzisha vyanzo vya ndani vya mapato pamoja na kubuni miradi ya ndani itakayowasaidia kuingiza mapato ya ndani. “Mambo mengi tulikuwa tunaenda tu lakini semina ya leo imenisaidia na imenigusa sana, natoa shukrani zangu kwa wadau, Mkuu wa Wilaya, Shekimweri pamoja na Mkurugenzi wa Jiji kwa kubuni semina hii kwaajili yetu, kwasababu imetufundisha mambo mengi kama wenyeviti” alisema Zitatu.







MWISHO

Comments

Popular Posts

Mbunge Mavunde akabidhi Kompyuta kwa Kata 41 za Jiji la Dodoma

Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Majengo Dodoma watarajia makubwa Mradi wa TACTIC

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma