Tofauti kati ya kuboresha taarifa katika daftari la kudumu la mpiga kura na kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Zoezi
la kuhakiki na kuboresha taarifa katika daftari la kudumu la mpiga kura
lililofanyika tarehe 25 Septemba, 2024 hadi Oktoba 1, 2024 lilimtaka mwananchi
kwenda kuboresha taarifa zake katika daftari la kudumu la mpiga kura tofauti na
zoezi la sasa ambalo linamtaka mwananchi kujiorodhesha katika orodha ya mpiga
kura lililoanza tarehe 11 hadi 20 Oktoba, 2024 linalohitaji mwananchi kwenda
kuandikishwa kwenye orodha ya mpiga kura kwa lengo mahususi kabisa la kuchagua
viongozi ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa.
Ufafanuzi
huo ulitolewa na Balozi wa Shina Namba Sita, Mtaa wa Chang’ombe katika Kata ya
Ihumwa, Adawila Zakayo alipokuwa akifafanua kwa wananchi tofauti ya zoezi la
kuboresha taarifa katika daftari la kudumu la mpiga kura na kujiandikisha
katika orodha ya mpiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Zoezi
la kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura lilikuwa ni kwa ajili
ya mwakani katika Uchaguzi Mkuu kwa ajili ya kumchagua Diwani, Mbunge na Rais.
Hili zoezi la sasa hivi la kujiandikisha katika orodha ya mpiga kura ni kwa
ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mtaa ambapo tutamchagua mwenyekiti na wajumbe
wake” alifafanua Zakayo.
Alisema
kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakishindwa kutofautisha kati ya kuboresha taarifa
na kujiandikisha katika orodha ya mpiga kura. Changamoto hiyo imekuwa ni chanzo
cha muitikio mdogo wa watu kujitokeza kwenda kujiandikisha hivyo tunaendelea
kutoa ufafanuzi ili kuwasaidia wananchi wetu waweze kujiandikisha katika orodha
ya wapiga kura. “Baadhi ya watu wanachanganya juu ya kujiandisha ingawa Tume ya
Huru ya Taifa ya Uchaguzi imefanya jitihada kubwa ya kuhabarisha umma kuhusiana
na kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura. Watu wengine
hawajitokezi kwasababu wanajua zoezi hili linaloedelea la kujiandikisha ni kwa
ajili ya kuchukua vitambulisho. Lakini sio, lengo la zoezi hili lililoanza tarehe
11 Oktoba, 2024 ni maalumu kwa kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa” alisema
Zakayo.
Hata
hivyo, alitoa rai kwa wananchi ambao bado hawajapata uelewa wa matukio haya ya
uchaguzi kuwa waendelee kufuatilia vyombo vya habari kwa sababu vinaelimisha
kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na pia waendelee kusikiliza kwa umakini
matangazo ambayo yanapita mitaani kwao na kujitokeza kwa wingi kuandikishwa
katika orodha ya wapiga kura. “Mimi kama Balozi, nimechukua hatua na
kuwahamasisha wananchi kwa kupita nyumba kwa nyumba na kuwatofautishia kati ya
zoezi lililopita na hili la sasa la kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura.
Na pia ninawapigia simu wale ambao nina namba zao nawaambia waende
kujiandikisha” alisisitiza Zakayo.
Zoezi
lililofanyika Septemba 25 hadi 1 Oktoba, 2024 mwananchi alikuwa na jukumu la
kwenda kuboresha taarifa zake kwa yule ambaye amebadili makazi yake na
kujiandikisha kwa yule ambaye ametimiza umri wa miaka 18 likiwa maalum kwa ajili
ya Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na rais. Zoezi linalofanyika hivi sasa la
kujiandikisha katika orodha ya mpiga kura lilianza tarehe 11 na litamalizika
oktoba 20, 2024 ni kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo mwananchi
anatakiwa kujiandikisha katika eneo lake la makazi ili aweze kumchagua mwenyekiti
wa kijiji, kitongoji na wajumbe wa halmashauri.
MWISHO
Comments
Post a Comment